Fahamu namna ya kuishi na mpenzi anayependa Fedha!

Sunday, December 70 comments



Leo nimekuja na mada ambayo naamini itawagusa wengi. Msomaji wangu, kusaidia katika mapenzi ni jambo zuri tena lenye mantiki sana na si la upande mmoja. Linaweza kuwa kwa wote, kwa mwanaume au mwanamke. Ni kati ya nguzo muhimu katika mapenzi, lakini kwa bahati mbaya kuna wale ambao
wamekuwa na tabia ya kupenda sana fedha!!
Wanasema kwamba wenzi wanajuana kulingana na wanavyoishi, hivyo ni rahisi sana kumgundua mwenzako kama anapenda sana fedha au ni kweli ana tatizo linalohitaji msaada wako. Hii ni kasoro, lakini haimaanishi kwamba ndiyo sababu ya kuachana.

Katika mada hii ipo dawa ya namna ya kudumu katika mapenzi motomoto na mwenzio wa aina hii. Imekuwa ni kawaida kumsikia msichana akitamba mbele ya wasichana wenzake kwa kusema: “Mimi nina kibuzi changu bwana kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nakitosa tu, yaani nakichuna kama sina akili nzuri.”
Umewahi kukutana na maneno ya aina hii? NDIO au SIO

Bila shaka jibu ni ndiyo. Si hivyo tu, wapo wanaume pia ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama watajishughulisha.
Ninachotaka kusema ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na fedha, ukiona mpenzi wako anaweka fedha mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.

Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze ukweli kisha muangalie namna nyingine ya kumsaidia.
Itakuwa siyo busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana na hili ni kwa pande zote mbili.

Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe ‘out’, bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana fedha au laah.
Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka? Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu? Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba fedha kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo siyo ya msingi, mbinu zifuatazo ni muhimu kuzifuata. Twende tukaone.

MWELEZE UKWELI
Kama huna fedha wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile.
Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana fedha au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza ‘mizinga’ ili afaidi.

JENGENI KUSAIDIANA
Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa. Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya basi analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake.
Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna fedha zinavyokuwa hazitoshi na ataweza kubana matumizi.

ACHA UFUJAJI
Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa fedha kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa unazo!
Unachotakiwa ni kudhibiti mapema matumizi yako hata kama fedha itakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakushibishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri kumbe huna kitu.

BAKI NA HILI
Katika kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, bali kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku na wewe ukiwa na tatizo akusaidie.
Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga mizinga mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.

UNA MAONI GANI JUU YA HILI
Share this article:

Unaonaje huu Muonekano?

 
Support : Management

Copyright © 2011. Al-amini Official blog - All Rights Reserved
Template Modify by Al-Amini
Proudly powered by Blogger